Bilioni 48 zatekeleza mradi wa vihenge Babati

0
111

Rais Samia Suluhu Hassan, leo amezindua mradi wa vihenge na maghala ya kuhifadhi nafaka wilayani Babati mkoani Manyara.

Mradi huo uliojengwa na mkandarasi Unia Sp. zo.o kwa kushirikiana na mkandarasi mzawa Elerai Construction Ltd, upo chini ya Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA).

Utekelezaji wa mradi huo umegharimu dola milioni 20.855 za kimarekani ambazo ni sawa na shilingi bilioni 48.175, na una uwezo wa kuhifadhi tani elfu 40 za nafaka.

Ulianza kujengwa mwezi Januari mwaka 2019 na kukamilika mwezi Juni mwaka huu, na utaendelea kuwa chini ya uangalizi wa mkandarasi kwa muda wa mwaka mmoja.

Mradi huo wa vihenge na maghala ya kuhifadhi nafaka wilayani Babati ni sehemu ya mradi mkubwa unaotajwa kuwa na uwezo wa kulisaidia Taifa kuongeza uwezo wa kuhifadhi tani laki mbili na nusu za nafaka hadi tani laki tano kwa gharama ya dola za kimarekani milioni 55.