Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Godwin Mollel amesema, Serikali imetenga shilingi bilioni 4.2 ili kuimarisha upatikanaji wa hewa tiba ya Oksijeni.
Akizungumza na waandishi wa Habari jijini Arusha kuhusu kampeni ya Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya UVIKO -19 Dkt. Mollel amesema kuwa, fedha hizo zitatumika kusimika mitambo ya kuzalisha hewa tiba ya Oksijeni, manunuzi ya mitungi, vifaa wezeshi pamoja na mfumo utakaowezesha uzalishaji wa hewa hiyo kwa wagonjwa wanaotibiwa katika hospitali mbalimbali nchini.
Kwa mujibu wa Dkt. Mollel, fedha hizo zitatumika kusimika mitambo Saba ya kuzalisha hewa tiba ya Oksijeni katika hospitali za kanda, hospitali maalum na hospitali za wilaya.
Amesema hatua hiyo itaongeza idadi ya mitambo ya kuzalisha hewa tiba ya Oksijeni kutoka 44 na kufikia 51.
Dkt. Mollel ametoa kauli hiyo zikiwa zimepita siku chache baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kuzindua kampeni ya Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya UVIKO -19, kampeni iliyozinduliwa jijini Dodoma.