Rais Samia Suluhu Hassan ametoa shilingi bilioni 21 kukamilisha mradi wa maji wa Kigamboni – Kimbiji wilayani Kigamboni mkoa wa Dar es Salaam na hivyo kuwezesha wananchi wa maeneo hayo kuanza kupata huduma ya maji safi na salama.
Akiwasha pampu ya kisima cha maji inayopeleka maji kwenye tenki la lita milioni 15, mkuu wa wilaya ya Kigamboni, Fatma Nyangasa ameipongeza Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) kwa kutekeleza mradi huo.
” Tunamshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa maamuzi ya kuiongezea nguvu DAWASA na kuwapa shilingi bilioni 21 ambapo matunda yake tunayafurahia baada ya kuwasha pampu ya kwanza, kisima cha kwanza na visima vingine 7 vipo tayari ni kiashiria kizuri kwa wanakigamboni kwamba sasa tunaenda kupata maji safi.” amesema Nyangasa
Kwa upande wake Mtendaji mkuu wa DAWASA Mhandisi Cyprian Luhemeja amesema serikali imeandika historia kwa kutekeleza mradi huo uliochukua takribani miaka nane kukamilika.
Mradi huo wa maji wa Kigamboni – Kimbiji utawanufaisha wakazi laki mbili na nusu wanaoishi katika kata tisa za wilaya ya Kigamboni.