Bilioni 1.6 kujenga VETA Chunya

0
262

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema Serikali imeamua kujenga vyuo vya ufundi stadi nchini, ili Wananchi hasa Vijana wapate ujuzi na ufundi wa aina mbalimbali utakaowawezesha kujiajiri na kuajiriwa.
 
Kauli hiyo imetolewa wilayani Chunya mkoani Mbeya na Waziri Mkuu Majaliwa, baada ya kukagua na kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa chuo cha ufundi stadi cha wilaya hiyo.
 
Amesema vyuo hivyo vya ufundi stadi vinajengwa ili kufungua milango ya ajira, kwa kuwa mafunzo yanayotolewa yatawawezesha wahusika kujiari kutika sekta mbalimbali ikiwemo ya viwanda.
 
 
Waziri Mkuu Majaliwa ameagiza ujenzi huo wa chuo cha ufundi stadi cha wilaya ya Chunya ukamilike kwa wakati, ili malengo ya Serikali ya kuhakikisha Wananchi wanapata elimu ya ufundi chuoni hapo yanafikiwa.
 
 
Pia ameuagiza uongozi wa mkoa wa Mbeya uhakikishe katika eneo la kijiji cha Mbugani kinapojengwa chuo hicho kunakuwa na huduma zote za kijamii zitakazotosheleza matumizi ya eneo hilo ikiwa ni pamoja na maji safi na salama na umeme.  
 
 
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) Dkt. Pancras Bujulu amesema mradi huo wa ujenzi wa chuo cha ufundi stadi wilayani Chunya una jumla ya majengo 17,  na utakapokamilika  chuo kinatarajiwa kuanza na fani sita za muda mrefu.
 
 
Gharama za ujenzi wa chuo hicho ni shilingi bilioni 1.6.