Bilioni 1.6 kuchagiza Taifa Stars kufuzu kombe la Dunia

0
255

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ametoa wito kwa watanzania pamoja na wadau wa soka nchini kuungana kwa pamoja na kuhakikisha timu ya Taifa ya Tanzania ya mpira wa Miguu (Taifa Stars), inafanya vizuri kwenye michezo yote iliyobaki ili kufuzu kushiriki kombe la Dunia litakalofanyika nchini Qatar 2022.

Ametoa wito huo leo (Alhamis, Novemba 4, 2021) wakati akiongoza kikao cha pamoja cha wadau wa soka nchini katika ukumbi wa uwanja wa Taifa wa Uhuru, Dar es Salaam. Katika kikao hicho wadau wa Taifa Star wamechangia Shilingi Bilioni 1.6 ambazo zitatumika kuihudumia timu katika maandalizi ya mechi zilizobaki za kufuzu kombe la Dunia.

Akizungumza kwenye kikao hicho, Waziri Mkuu amesema ni lengo la Rais Samia Suluhu Hassan kuhakikisha anakuza sekta ya michezo nchini na anataka kuona mafanikio katika timu za Taifa hivyo mikakati ya kuifanya timu ya Taifa ifanikiwe ni sehemu ya kutimiza malengo ya Rais.

Katika hatua nyingine Waziri Mkuu ametoa wito kwa wamiliki wa viwanda, Taasisi za Umma na binafsi pamoja na wadau wengine kuendelea kujitokeza kuichangia timu ya Taifa ili iweze kuweka Historia ya kushiriki kombe la dunia kwa mara ya kwanza.

Wadau Walioshiriki katika kikao hicho ni pamoja na GSM, TAIFA GAS, AZAM, CRDB, NBC, LAKE OIL, STAR OIL, K4 SECURITY, KAMBIASO pamoja na wadau wengine.