Bilioni 1.1 zajenga vyumba vya madarasa 53 Misenyi

0
177

Waziri wa TAMISEMI, Innocent Bashungwa amesema Serikali kupitia fedha za IMF imetoa shilingi bilioni 1.1 kwa ajili ya ujenzi wa madarasa 53 ya shule za sekondari na milioni 200 za kujenga madarasa 10 ya shule shikizi katika Halmashauri ya Wilaya ya Misenyi mkoani Kagera.

Ameyasema hayo wakati akitoa salamu katika Ziara ya Makamu wa Rais, Dkt. Philip Mpango wakati wa uzinduzi wa jengo ya kitega uchumi cha Shirika la Nyumba la Taifa kilichopo Mutukula Misenyi, Kagera.

Waziri Bashungwa amesema kwa Mwaka wa fedha wa 2021/ 22 Halmashauri ya wilaya Misenyi imeshapokea Milioni 695 kuendeleza sera ya elimu bila malipo katika shule za msingi na sekondari katika Halmashauri hiyo.

Amesema kupitia Mpango wa Uboreshaji wa Elimu ya Sekobdari (SEQUIP) Serikali imetoa shilingi milioni 470 za ujenzi wa shule mpya za sekondari katika kata ambazo hazikuwa na shule za sekondari za kata.

Aidha, Waziri Bashungwa ameeleza kuwa milioni 262.5 zimetolewa kukamilisha vyumba vya madarasa vya shule za msingi na Sekondari ambapo madarasa 12 ya shule za sekondari na madarasa 9 ya shule za msingi sambamba na milioni 150 za ujenzi wa maabara 6 za sekondari.

Ametoa wito kwa Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt Angeline Mabula kupitia shirika la Nyumba la Taifa kukutana na kuweka mpango wa kujenga masoko na stendi za kisasa katika Halmashari na kuweka ubia wa Ofisi ya Rais – TAMISEMI  kulipa kwa awamu.