Bil 7 kukamilisha ujenzi wa daraja Berega

0
234

Serikali kupitia Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA), inaendela na ujenzi wa daraja jipya la Berega wilayani Kilosa mkoani Morogoro.

Ujenzi wa daraja hilo utagharimu shilingi bilioni saba hadi kukamilika kwake.

Akizungumza wakati wa ziara ya kukagua miradi inayotekelezwa na TARURA, Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya wakala huo Mhandisi Florian Kabaka amesema ujenzi wa daraja hilo utaleta manufaa kwa wananchi wa Berega na maeneo mengine waliokuwa wakipata adha ya usafiri baada ya daraja la awali kuvunjika .

Amesema kuwa daraja hilo litawaunganisha wananchi wa Morogoro na maeneo mengine kama Gairo, Dodoma na Tanga.

Kwa upande wake Mhandisi Benjamini Maziku ambaye ni Kaimu meneja wa TARURA mkoa wa Morogoro amesema kuwa, daraja hilo litakuwa na uwezo wa kupitisha magari ya aina yote, hivyo kuwarahisishia wananchi usafiri na usafirishaji wa mazao.

Mradi wa Ujenzi wa Daraja la Berega unahusisha ujenzi wa daraja lenye urefu wa mita 140, barabara za mkaribio za daraja mita 600 na maboresho ya barabara kutoka Berega kwenda Dumbalume kilometa saba katika Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa.