Benki ya Biashara Tanzania katika kipindi cha robo ya mwaka huu wa 2024 imetengeneza faida ya shilingi Bilioni 10.7 baada ya kodi.
Faida hiyo ni ongezeko la asilimia 529 ikilinganishwa na shilingi Bilioni 1.7 kwa kipindi kama hicho kwa mwaka 2023, huku ikitarajia kukusanya zaidi ya shilingi Bilioni 40.
Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo Adama Mihayo amesema hayo mkoani Dar es Salaam wakati wa mkutano wa wahariri na waandishi wa habari.
Amesema faida kabla ya kodi ilikuwa shilingi Bilioni 13.6 kwa kipindi cha robo ya kwanza ya mwaka huu ambayo ni sawa na asilimia 353 ukilinganisha na shilingi Bilioni tatu.
Mapato ya Benki ya Biashara Tanzania kwa kipindi cha robo ya kwanza ya mwaka 2024 yamefikia shilingi Bilioni 56.8 kutoka shilingi Bilioni 43.7 Kwa kipindi kama hicho mwaka 2023.