Benki ya Equity kuwekeza trilioni 13

0
130

Naibu Katibu Mkuu wa wizara ya Fedha na Mipango Lawrence Mafuru ameihakikishia benki ya Equity kwamba Tanzania iko tayari kushirikiana na benki hiyo kutekeleza mpango mkakati utakaowezesha upatikanaji wa zaidi ya shilingi trilioni 13 zilizopangwa kutolewa na benki hiyo kuendeleza mipango mbalimbali ya maendeleo kikiwemo kilimo katika nchi za Afrika Mashariki.

Mafuru amesema hayo jijini Dodoma alipokutana na kufanya mazungumzo na ujumbe wa benki hiyo yenye makao makuu yake nchini Kenya.

Amesema kuwa benki hiyo imedhamiria kuwekeza fedha katika maeneo sita ikiwemo sekta za kilimo, madini, uendelezaji wajasiliamali wadogo na wa kati, mazingira, utawala bora, viwanda na sekta ya biashara.

Mafuru amesema uwekezaji huo utagusa maeneo mbalimbali ya kiuchumi ikiwemo kukuza ajira na kuviwezesha viwanda vilivyoko katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki kupata malighafi na soko la uhakika hususan baada ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo kujiunga na Jumuiya hiyo.

Akizungumza kwa niaba ya ujumbe wa benki hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa benki ya Equity kwa upande wa Tanzania, Isabela Maganga amesema benki hiyo inataka kushirikiana na Serikali kukuza uchumi wa nchi na kuwawezesha wananchi kiuchumi.

Amesema uwekezaji wa shilingi trilioni 13 unaotaka kufanywa na benki hiyo katika nchi za Afrika Mashariki ikiwemo Tanzania, utakuwa wa kipindi cha miaka mitano ambapo watatoa mikopo kwa watu milioni 5 na kuzalisha ajira milioni 50.