Benki ya Dunia yakagua miradi Tanzania

0
242

Wawakilishi wa Benki ya Dunia nchini Tanzania leo wamefanya ziara ya siku moja kukagua miradi inayofadhiliwa na Mfuko wa Kuendeleza Ujuzi (SDF) unaoendeshwa na Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ambapo Mfuko huo unaratibiwa na Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA).

Katika ziara hiyo, wawakilishi hao, Xiayon Liang na Innocent Mulindwa  wamekagua miradi miwili kati ya 81 inayotekelezwa katika awamu ya pili ya utekelezaji wa SDF ambapo wametembelea mradi wa kuendesha na kutengeneza pikipiki za magurudumu matatu na mawili unaotekelezwa na Chuo cha Mafunzo na Ufundi Stadi cha Future World kilichopo eneo la Gongolamboto. Taasisi hiyo ilipata ufadhili wa shilingi milioni 128.9 ambapo vijana 415 wamenufaika na mafunzo yaliyotolewa kupitia ufadhili huo wa SDF.

Mradi mwingine uliotembelewa ni mradi wa Mafunzo ya Mafundi wa Matengenezo ya Simu, unaoendeshwa na Chuo cha Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) katika fani ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA). Chuo hicho kilichopo eneo la Kipawa kilipata ufadhili wa shilingi milioni 128.8 ambapo vijana 476 wamenufaika na ufadhili huo wa mfuko wa SDF.

Katika awamu ya kwanza ya mradi ulioanza kutekelezwa katika mwaka wa fedha 2018/2019 Taasisi 15 zilifadhiliwa kwa jumla ya shilingi bilioni 3.1 wakati katika awamu ya pili Taasisi 81 zimenufaika kwa ufadhili wa kiasi cha shilingi bilioni 9.7 kuendesha programu za mafunzo ya ujuzi.