Benki ya Dunia kufadhili miradi zaidi ya elimu

0
881

Rais John Magufuli amekutana na kufanya mazungumzo na mkurugenzi mkazi wa Benki ya Dunia hapa nchini Bella Bird, mazungumzo yaliyohusu maendeleo ya miradi inayofadhiliwa na benki hiyo.

Baada ya mazungumzo hayo Bella Bird amesema kuwa miradi inayotekelezwa kwa ufadhili wa Benki ya Dunia nchini  Tanzania imefikia thamani ya shilingi Trilioni 10.186 na kwamba maendeleo ya miradi hiyo ni mazuri.

Ameongeza kuwa kwa sasa wanakamilisha maandalizi ya ufadhili wa miradi mingine inayohusu sekta ya elimu hasa elimu ya awali na sekondari itakayogharimu shilingi Trilioni 1.357 na kwamba maandalizi hayo yatakamilika mwezi Novemba mwaka huu.

“Kwa hiyo nimekutana na Mheshimiwa Rais Magufuli kuzungumzia maendeleo ya miradi hiyo na kwa ujumla maendeleo ni mazuri” amesema mkurugenzi mkazi huyo wa Benki ya Dunia hapa nchini Bella Bird.