Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) imetangaza ongezeko la bei za mafuta ya petroli, dizeli na mafuta ya taa yanayoingia nchini kupitia bandari ya Dar es salaam.
Mabadiliko hayo ya bei ya mafuta kwa wanunuzi wa jumla na rejareja yanayoanza hii leo, yametokana na ongezeko la bei ya mafuta katika soko la dunia na gharama za usafirishaji.
Taarifa ya EWURA kwa vyombo vya habari imeeleza kuwa, bei za rejareja kwa mafuta ya petroli na dizeli zimeongezeka kwa shilingi 142 na shilingi 85 kwa lita, huku bei ya jumla ikiongezeka kwa shilingi 141.92 na shilingi 84.95 kwa lita.
Ongezeko hilo la bei linamaanisha kuwa, kwa sasa wakazi wa Dar es salaam watanunua lita moja ya petroli kwa shilingi 2,123 na dizeli kwa shilingi 1,996 kutoka shilingi 1,981 na shilingi 1,911 waliyokuwa wakinunua mwezi uliopita.
Mabadiliko ya bei hizo pia yamegusa mikoa ya Tanga, Kilimanjaro, Arusha na Manyara ambapo bei za rejareja za petroli na dizeli zimeongezeka kwa shilingi 73 na shilingi 105 kwa lita.
Pia bei ya jumla ya petroli na dizeli katika mikoa hiyo imeongezeka kwa shilingi 72.38 na shilingi 105.12, huku bei ya mafuta ya taa ikiendelea kusalia kama ilivyokuwa katika toleo la Machi 3 mwaka huu.
Kwa mujibu wa taarifa ya EWURA, kufuatia mabadiliko hayo ya bei za mafuta ya petroli, dizeli na mafuta ya taa, kampuni za mafuta ziko huru kuuza bidhaa za mafuta kwa bei ya ushindani mradi tu bei hizo zisivuke bei kikomo kama ilivyokokotolewa na kanuni iliyopitishwa na Mamlaka hiyo.