Bashungwa: Kigamboni – Magogoni kuna figisu

0
108

Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa amesema wamekuwa wakifanya vikao na mamlaka husika ili kuboresha usafiri wa vivuko kati ya Kigamboni na Magogoni mkoani Dar es Salaam, huku akisisitiza kwamba kumekuwa na figisu kutoka kwa baadhi ya watu kwa ajili ya maslahi binafsi.

Akizungumza na TBC kupitia kipindi cha Jambo Tanzania, Waziri Bashungwa amewatoa hofu wakazi wa Kigamboni na Dar es Salaam kwa ujumla kwamba Serikali inafanyia kazi suala hilo, na ndani ya muda mfupi changamoto hiyo itakwisha na watavuka kwa muda mfupi zaidi.

“Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan tumejipanga vizuri kuhakikisha tunaboresha vivuko na tutatoa machaguo ambapo abiria ataweza kuamua kupanda kivuko cha TEMESA au Sea Tax za Azam,” amesema.

Amesema hadi Agosti mwaka huu utaratibu huo utakuwa kwenye hatua za utekelezaji, huku akisema kuwa kuna watu wanashinikiza mambo yaende kama wanavyotaka wao, lakini hilo haliwezekani.

Aidha, Waziri Bashungwa amesema kwa sasa makandarasi wazawa wanatekeleza asilimia 96 ya kazi zote za ujenzi wa barabara nchini lakini thamani ya kazi zao ni asilimia 40, huku makandarasi wa kigeni wakiwa na kazi chache lakini zinazobeba asilimia 60 ya thamani ya miradi yote.

Kutokana na hilo, ameweka bayana kuwa wizara imekutana na kujadiliana na makandarasi wazawa ili kutatua changamoto zao, hasa za kifedha, ili nao waweze kutekeleza miradi mikubwa, mkakati unaokwenda pamoja na kauli mbinu ya maonesho inayosema “Taifa ni Ujenzi, Tulijenge Pamoja.”