Ubadhirifu wa fedha wa shilingi bilioni 3.93 umebainika katika katika bandari za Mwanza na Kigoma.
Katika bandari ya Mwanza, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) amebaini ubadhirifu wa shilingi bilioni 3.27 zilitolewa katika akaunti ya benki ya Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) iliyopo CRDB kupitia miamala 737.
Akitoa taarifa kwa Waandishi wa habari jijini Dodoma kuhusu ukaguzi wa mashirika ya umma kwa mwaka wa fedha wa 2019/2020, CAG Kichere amesema kuwa malipo ya fedha hizo hayakuwa na hati za malipo na pia matumizi yake hayakuoneshwa katika taarifa za fedha.
Katika Bandari ya Kigoma, Kichere amesema shilingi milioni 655.90 zilitolewa kutoka benki kwa kutumia hundi 30 bila kuwa na hati za malipo kuthibitisha malipo yaliyofanywa, na hundi hazikusajiliwa kwenye daftari la udhibiti wa hundi, na vipande vitano vya hundi havijaonekana katika daftari la udhibiti wala katika taarifa za benki .
Halkadhalika, katika bandari hiyo ya Kigoma, CAG amebaini ukosefu wa ripoti za mapato za kila siku ili kuhakiki ripoti za mapato ya kila mwezi kwa kipindi cha miezi 7, hali inayoweza kusababisha upotevu wa fedha za Serikali ikiwa fedha hazitarejeshwa.
Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu huyo wa Hesabu za Serikali amependekeza TPA kwa kushirikiana na vyombo vya usalama, ihakikishe fedha zinapatikana na hatua za kisheria zinachukuliwa dhidi ya waliohusika.