Bandari ya Mtwara yaongeza uwezo kuhudumia mizigo

0
194

Shehena ya mizigo inayohudumiwa kupitia Bandari ya Mtwara imeongezeka kutoka wastani wa tani Laki nne hadi kufikia tani Milioni 1.6 iliyohudumiwa kwa mwaka wa fedha wa 2022/2023.

Ongezeko hilo linatokana na bandari hiyo kufanya uwekezaji wenye thamani ya shilingi Bilioni 157.8 katika maeneo mbalimbali ikiwemo eneo la gati, ununuzi wa mtambo wa kupakia na kushusha mizigo na kuimarishwa kwa mifumo ya bandari.

Akizungumza bandarini hapo baada ya kupokea Wahariri wa Habari kutoka Jukwaa la Wahariri nchini (TEF) Meneja wa Bandari ya Mtwara, Ferdinand Nyathi amesema kupitia msimu wa korosho ambao upo mwishoni bandari hiyo imehudumia meli kubwa 28.

Amesema mizigo mingine iliyohudumiwa kupitia bandari hiyo ni pamoja na makaa ya mawe na saruji ya kiwanda cha Dangote ambayo husafirishwa kutoka Mtwara kuelekea Zanzibar na Comoro.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Masoko na Uhusiano kutoka Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) Dkt. George Fasha amesema mpango uliopo sass ni bandari hiyo kuanza usafirishaji wa madini ya Graffite kutoka Ruangwa na kwamba ili kuimarisha Ushoroba wa Kusini Mamlaka hiyo inaendelea kuimarisha bandari ya Bambabay ili iweze kusaidia Bandari ya Mtwara kuhudumia shehena kubwa ya mizigo kuelekea nchi za Malawi na Msumbiji.