Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji na Mitaji ya Umma imesema kuwa Bandari ya Dar es Salaam ina uwezo mdogo wa kupokea mizigo ukilinganisha na uwezo wa reli ya kisasa (SGR) iliyoigharimu Serikali kwa uwekezaji mkubwa ilihali bandari hiyo ni chanzo kikuu cha mizigo.
Hayo yamesemwa bungeni jijini Dodoma na Mwenyekiti wa kamati hiyo, Jerry Silaa wakati akitoa hoja ya kamati iliyotokana na ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu ya Serikali kwa mwaka wa fedha wa 2020/2021.
Kamati imeliambia bunge kuwa hali hiyo itachangia SGR isipate mzigo wa kutosha kwa ajili ya kusafirishwa pindi itakapokamilika, hivyo kukwamisha kupatikana kwa tija ya uwekezaji uliofanyika.
Hivyo, Bunge limeazimia kwamba Serikali iharakishe utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa bandari ya Bagamoyo, pia iharakishe zoezi la kuongeza ufanisi wa bandari ya Dar es Salaam ikiwa ni pamoja na kuongeza gati za kisasa katika Bandari ya Dar es Salaam na zoezi hilo kikamilike kabla ya ujenzi wa reli ya SGR kukamilika.
Bunge limesema kuwa hatua hiyo itasaidia SGR kupata mizigo ya kusafirisha hivyo kuleta tija
iliyokusudiwa.