Bandari Mtwara yazidi kujiimarisha kivifaa

0
320

Bandari ya Mtwara imepokea boti maalumu kwa ajili ya kusaidia meli kutia nanga na kuondoka kwenye gati mara baada ya kushusha au kupokea mizigo.

Boti hiyo maarufu kama Tugboat yenye thamani ya shilingi bilioni 25 imenunuliwa na Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) kutoka nchini Vietnam kufuatia agizo la Rais Samia Suluhu Hassan la kuhakikisha Bandari ya Mtwara inakuwa na vifaa vyote vya muhimu kwa ajili ya kurahisishia shughuli za kibandari.

Tugboat ni boti maalumu za kuvuta meli katika hali ambayo haziwezi au hazipaswi kusogea chini ya uwezo wao zenyewe kutokana na mazingira ya bandari.

Akizungumza mara baada ya kupokea boti hiyo, Kaimu Maneja wa Bandari ya Mtwara, Sudi Mwarabu amesema ujio wa boti hiyo utaongeza na kuleta ufanisi katika utendaji kazi wa bandari hiyo katika kupokea shehana kubwa za mizigo.

Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Kanali Patrick Sawala amesema serikali imewekeza miundombinu ya kisasa katika bandari ya Mtwara ili kuongeza uwezo wa kuhudumia shehena kubwa.