Balozi wa China, Wang Ke aondoka nchini

0
199

Raia Samia Suluhu Hassan amemshukuru Balozi wa China nchini anayemaliza muda wake Wang Ke kwa jitihada zake za kuendeleza na kukuza uhusiano wa Tanzania na China, ambao umewezesha kutekelezwa kwa miradi mbalimbali iliyofadhiliwa na China hapa nchini.

Rais Samia Suluhu Hassan ametoa shukrani hizo Ikulu Chamwino mkoani Dodoma, wakati wa mazungungumzo yake na Balozi Wang Ke Ikulu Chamwino mkoani Dodoma ambapo alifika kwa ajili ya kuaga.

Amesema akiwa hapa nchini Balozi Wang Ke amewezesha kutekelezwa kwa miradi mbalimbali inayofadhiliwa na China nchini ikiwa ni pamoja na maktaba ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, jengo la Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki lililopo jijini Dar es salaam na msaada wa shilingi bilioni 35 zilizoelekezwa katika miradi ya maendeleo.

Rais Samia Suluhu Hassan kupitia kwa Balozi Wang Ke pia ameishukuru China kwa ufadhili wa miradi mbalimbali ya ujenzi wa miundombinu na uboreshaji wa huduma za kijamii pamoja na ushirikiano wa kibiashara na uwekezaji ambao pamoja na kukuza pato la nchi umesaidia Watanzania wengi kupata ajira.

Amepokea salamu za Rais wa Xi Jinping wa China na amemtakia yeye na Wachina wote maadhimisho mema ya miaka 100 ya Chama cha Kikomunisti cha China (CPC) yatakayofanyika Julai, 2021 Mosi mwaka huu.

Kwa upande wake Balozi Wang Ke amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa ushirikiano mkubwa alioupata kutoka serikalini wakati wote wa kipindi chake cha Ubalozi.

Amewasilisha kwa Rais Samia Suluhu Hassan salamu za Rais Xi Jinping wa China, ambaye amesema ana imani kubwa kuwa atafanya mazuri kwa Tanzania kutokana na dhamira yake ya kuendeleza kazi nzuri iliyofanywa na aliyekuwa Rais wa Tanzania Hayati Dkt. John Magufuli.

Aidha, Balozi Wang Ke amesema China ipo tayari kushirikiana na Tanzania katika kukabiliana na ugonjwa wa corona.