Mradi wa kuongeza wakunga vijijini waokoa maisha ya mama na mtoto

0
222

Balozi wa Canada nchini Pamela O’donnel ameshauri kuendelezwa kwa mafanikio yaliyopatikana katika mradi wa kuongeza wakunga bora vijijini ikiwemo kupunguza vifo vya mama wajawazito na watoto wachanga katika mikoa ya Kanda ya Ziwa na Magharibi.

Balozi O’donnel ametoa wito huo wakati wa kuhitimisha mradi huo uliofadhiliwa na Serikali ya Canada kwa gharama ya shilingi billioni 16 na kuhusisha maboresho ya miundombinu katika vyuo 20 na hospitali zinazotoa mafunzo ya uuguzi na ukunga katika kanda hizo pamoja na kujenga maabara za kufundishia katika vyuo hivyo.

Mradi wa kuongeza wakunga bora vijijini uliotekelezwa taasisi isiyo ya kiserikali ya JHPIEGO unaelezwa kuleta matokeo chanya katika mikoa minane ya Kanda ya Ziwa na Magharibi ikiwemo kupunguza vifo vya mama wajawazito na watoto wachanga.

Maboresho hayo yamewezesha wataalamu 2,037 kuhitimu uuguzi na ukunga kwenye vyuo hivyo tangu mwaka 2016 hivyo kupunguza uhaba wa wataalam hao kwa asilimia 13 katika maeneo yasiyofikika kwa urahisi.

Mradi huo uliotekelezwa kwa miaka mitano umehitimishwa jijini Mwanza na Mkurugenzi wa Idara ya Kinga Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto, Dkt. Leonard Subi.