Balozi Kanza: Tanzania itashirikiana na mtu yoyote

0
169

Balozi wa Tanzania nchini Marekani Dkt. Elsie Kanza amesema, sera ya Tanzania ni kushirikiana na kila mtu ilimradi aheshimu mila na desturi za nchi na haibagui Taifa lolote.

Akizungumzia ziara ya Makamu wa Rais wa Marekani Kamala Harris hapa nchini, Balozi Kanza amesema, ziara hiyo ni matokeo ya ziara ya Rais Samia Suluhu Hassan nchini Marekani na kwamba imeangalia maeneo mbalimbali ikiwa ni pamoja na uimarishaji wa ushirikiano baina ya mataifa hayo mawili.

Dkt. Kanza amesema, Tanzania imekuwa na ushirikiano na mataifa mbalimbali na ziara ya Makamu wa Rais wa Marekani hapa nchini ni matokeo ya ushirikiano, heshima na urafiki uliodumu kwa muda mrefu.

Balozi Kanza amesema kuwa, Ubalozi wa Tanzania nchini Marekani unafuatilia mikataba yote inayoingiwa baina ya Wawekezaji wa Marekani na Tanzania, ili kuwawezesha kufikia malengo yao ya uwekezaji hapa nchini.

Kuhusu maadili baina ya nchi hizo mbili Balozi Kanza amesema, kila Taifa lina heshimu mila na desturi za Taifa lingine, hivyo hakutakuwa na muingiliano wowote baina ya Mataifa hayo mawili.

Balozi Kanza alikuwa akizungumza katika kipindi cha Jambo Tanzania, kinachorushwa hewani na TBC 1.