Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Kusini Unguja imemfukuza uanachama mwanachama mkongwe wa chama hicho, Balozi Ali Abeid Karume kutokana na mwenendo wake wa kukiuka maelekezo ya maadili, miongozo na nidhamu iliyoainishwa katika Katiba ya CCM ya mwaka 1977 toleo la mwaka 2022.
Akizungumza mara baada ya kutolewa maazimio ya kikao hicho Katibu wa Siasa na Uenezi wa CCM mkoa huo, Ali Timamu Haji amesema uamuzi huo umefikiwa kwa mujibu wa Katiba ya CCM ya mwaka 1977 toleo la mwaka 2022 ibara ya 89 inayoeleza kazi za Halmashauri Kuu ya Mkoa inayoelekeza kuangalia mienendo ya wanachama na viongozi wa CCM wa ngazi ya mkoa kichama na kulazimika kutoa taarifa kwa vikao vinavyohusika ngazi za juu.
Pia, Ibara ndogo ya 14 kifungu kidogo cha 14 kinaelekeza kumuachisha au kumfukuza uanachama mwanachama yeyoye endapo itathibitika kwamba tabia na mwenendo wake vinamwondolea sifa za uanachama wake na mwanachama anayeachishwa au kufukuzwa uanachama anaweza kukata rufaa kwa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa.
Balozi Karume ametakiwa kurudisha kadi ya uanachama wa CCM ya kielektroniki namba C000/2809/993/1 ya tarehe 17/03/2022.
“Mwanachama huyu ameitwa na kuonywa kwa maandishi na vikao mbalimbali vya Chama Cha Mapinduzi, lakini hakutii wala kubadilisha tabia na vitendo vyake na kuendelea kukiuka kwa makusudi maadili na miongozo ya CCM, hivyo kwa mamlaka tuliyopewa na katiba yetu, ngazi ya Mkoa wa Kusini Unguja kwa kauli moja tumefikia maamuzi makubaliano ya kumuachisha na kumfukuza uanachama mwanachama huyo,’’ amefafanua Ali Timamu Haji
Balozi Ali Abeid Karume ni mtoto wa kwanza wa Rais wa Kwanza wa Zanzibar, Mzee Abeid Amani Karume pia ni ndugu wa Rais Mstaafu wa awamu ya sita wa Zanzibar, Amani Abeid Karume.