Madaktari wa Hospitali ya Taifa Muhimbili wamefanikiwa kumtoa pini kwenye mapafu mtoto mwenye umri wa miaka mitano kwa kutumia kifaa maalum chenye kamera kilichopelekwa moja kwa moja hadi ilipo, kuinasa na kisha kuitoa pini hiyo ambayo amekaa nayo kwa takribani mwezi mmoja.
Wazazi wa mtoto huyo wakazi wa Dar es Salaam wamesema mtoto wao alianza kupata kikohozi na homa za mara kwa mara na walipompeleka kwenye hospitali moja binafsi alifanyiwa baadhi ya vipimo vilivyoonesha uwepo wa maambukizi kifuani.
Siku iliyofuata alifanyiwa kipimo cha X-Ray na kugundulika ana pini ya kubandikia matangazo ambayo madaktari walijaribu kuitoa bila mafanikio na kuwashauri wampeleke Kenya au Afrika ya Kusini ili ikatolewe.
“Kabla ya kufikia uamuzi wa kumpeleka Kenya au Afrika Kusini mume wangu alisema aliona “clip” kwenye vyombo vya habari kuwa Hospitali ya Taifa Muhimbili hivi karibuni ilifanikiwa kumtoa mtoto Skrubu (Screw)…hivyo tuliomba tupewe rufaa kuja Muhimbili ambayo tulipewa na kupokelewa vizuri hapo Emergency ya Muhimbili ambao walimfanyia X-Ray na kuona pini ilipokaa na kutuambia kuwa mtoto wanamlaza na atafanyiwa procedure ya endoscope kesho yake,” Amesema mama wa mtoto huyo.
Amesema huduma ya kumtoa pini mtoto huyo ilifanyika kwa mafanikio na kwa sasa hakohohi tena na anaendelea vizuri.