Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi imeiagiza Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL) kufanya uchunguzi wa nauli zinazotozwa na mashirika washindani katika safari za ndani, na kuweka nauli ambazo zitawavutia Watanzania wengi zaidi kutumia ndege zao.
Agizo hilo limetolewa na Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Godfrey Kasekenya wakati akijibu swali la Mbunge wa Gando, Salim Mussa Omari aliyetaka kujua nini kinasababisha mabadiliko makubwa ya bei za tiketi za ATCL kwa safari za Dar es Salaam na Dodoma ambapo mara nyingi hufika hadi shilingi laki sita.
Naibu Waziri ameeleza kwamba uuzaji wa tiketi katika biashara ya usafiri wa anga ni moja ya mikakati ya ushindani ili kuvutia wateja ambapo tiketi hupangwa kwa ngazi mbalimbali kizingatia vigezo kama bei ya tiketi, ujazo wa ndege, muda wa kukata tiketi masharti ya tiketi na daraja la tiketi.
“Mteja ambaye anataka tiketi mapema na kukuta ndege haijajaa, hupata tiketi kwa bei ya chini, ikilinganishwa na mteja anayekata tiketi yake muda mfupi kabla ya safari na kukuta ndege imejaa, hupata bei ya juu,” ameeleza.
Kasekenya amesema kwa safari za Dar es Salaam na Dodoma, kwenda na kurudi, ATCL ina ngazi 13 katika daraja la kawaida (economy class) ambapo bei zake zinaanza shilingi 331,400 hadi 678,400. Ameongeza kuwa kuna kuna daraja la biashara (business class) ambalo lina ngazi tatu zenye huduma maalum na nauli zake ni kati ya shilingi 721,600 hadi 953,000.
Licha ya maelezo hayo, ATCL imeagizwa kufanya mapitio na kupanga nauli zinazoweza kuwavutia Watanzania kutumia ndege hizo.