Mkuu wa mkoa wa Mtwara Brigedia Jenerali Marco Gaguti amesema atamchukulia hatua za kisheria mtu yeyote atakayejihusisha na hujuma kwenye zao la korosho, katika kipindi hiki ambapo minada ya ununuzi wa zao hilo inaendelea.
Brigedia Jenerali Gaguti ametoa kauli hiyo baada ya kutembelea ghala kuu la kuhifadhia korosho la chama kikuu cha ushirika cha TANECU cha wilaya za Tandahimba na Newala, na kuongeza kuwa hatopenda kuona Taifa linaingia dosari kwa kusafirisha nje korosho ghafi zikiwa na kashfa ya kukosa ubora.
Akizungumza na baadhi ya Wakulima wa korosho waliokusanyika katika ghala hilo, Brigedia Jenerali Gaguti amedai kuwa kuna baadhi ya watu ambao hawana nia njema na Serikali kwa kutaka kuhujumu zao la korosho, hivyo ni vema wakaacha hujumu hizo vinginevyo wataishia pabaya.
Katika hatua nyingine mkuu huyo wa mkoa wa Mtwara amesema, njia sahihi ya kupunguza malalamiko kutoka kwa Wakulima kuhusu bei ya korosho ghafi ni kuanza kubangua korosho badala ya kuendelea kuuza zikiwa ghafi.
Tanzania ina viwanda 35 vya kubangua korosho, ambapo vinavyofanya kazi mpaka sasa ni vinane tu na vimekuwa vikibangua korosho chini ya asilimia 10 kati ya korosho zote zinazosafirishwa kwenda nje.ya nchi.