Rais John Magufuli ambaye anaendelea na ziara yake ya siku Nane mkoani Mbeya, hii leo anashiriki Ibada ya kumsimika Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Mbeya Mhashamu Askofu Gervas Nyaisonga.
Ibada hiyo inafanyika katika uwanja wa Sokoine jijini Mbeya na kuhudhuriwa na wageni mbalimbali.
Miongoni mwa shughuli alizofanya Rais Magufuli hapo jana akiwa katika ziara yake mkoani Mbeya, ni kufungua barabara ya lami ya Mbeya – Chunya na kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa barabara ya lami ya Chunya – Makongolosi, zote zikiwa ni sehemu ya barabara kuu ya Mbeya – Makongolosi – Rungwa yenye urefu wa kilometa 528.
Ujenzi wa barabara ya lami ya Mbeya – Chunya yenye urefu wa kilometa 72 umegharimu Shilingi Bilioni 140 na ujenzi wa barabara ya Chunya – Makongolosi uliopangwa kukamilika mwezi Januari mwaka 2020 utagharimu Shilingi Bilioni 62.7 na fedha zote zimetolewa na Serikali.
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS) Mhandisi Patrick Mfugale amesema kuwa barabara hizo ni sehemu ya barabara kuu ya Mbeya – Makongolosi – Rungwa yenye urefu wa kilometa 528 na kwamba ujenzi wa barabara ya Chunya – Makongolosi umefikia asilimia 33.2.