Askofu Mhasi: Tusiache mitandao ilee watoto

0
216

Katika kusherekea Sikukuu ya Pasaka, waumini wa dini ya Kikristo nchini wamekumbushwa kushirikiana katika malezi bora ya Watoto kwa kuwafuatilia hatua kwa hatua hata waweze kusikia sauti ya Mungu na kufanya maamuzi sahihi kwenye maisha yao.

Akitoa mahubiri mkoani Ruvuma katika Ibada ya Misa Takatifu ya Pasaka kitaifa katika Kanisa Kuu la Kiaskofu la Mtakatifu Francisco Xavery Jimbo Katoliki la Tunduru-Masasi, Askofu wa jimbo hilo Mhashamu Filbert Mhasi amesema ni wajibu wa Wazazi na Walezi nchini kuwa wa kwanza kwenye malezi ya watoto wao kabla ya jamii inayomzunguka kufanya hivyo.

” Serikali itakusaidia, jamii itakusaidia,lakini wewe kama mzazi uwe ni wajibu wako kumfuatilia mtoto wako hata katika mabadiliko yake, tusiawaache watoto walelewe na mitandao ya kijamii.” Amesisitia Askofu Mhasi

Pamoja na mambo mengine Askofu Mhasi amesema sherehe za Pasaka ni furaha, amani, matumani na amani, hivyo kuwataka waumini wa dini ya Kikristo nchini na Watanzania wote kujenga upendo wa kweli kwa wengine.

“Kuna watu wanahangaika kwa sababu ya kukosa mlo mmoja kwa siku, lakini pia wapo wanaohangaika kwa sababu ya kukata tamaa, kukosa ajira na changamoto ya dawa za kulevya, hivyo nawaalika wakati huu Pasaka kueneza furaha na upendo kwa watu wa aina hiyo kwenye jamii.” Amesisitiza Askofu Mhasi