Makamu wa Rais, Dkt. Philip Mpango amemwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan katika Ibada na sherehe ya Jubilei ya dhahabu ya miaka 50 ya Upadre wa Mhashamu Askofu Methodius Kilaini ambaye ni Askofu Msaidizi Jimbo Katoliki la Bukoba.
Akizungumza katika Kanisa Kuu Katoliki wilayani Bukoba mkoani Kagera Dkt. Mpango amesema Serikali inatambua na kushukuru mchango wa Baba Askofu Kilaini katika kanisa na jamii ya Watanzania.
Aidha amelipongeza na kulishukuru Kanisa Katoliki kwa kuunga mkono juhudi za Serikali na kwa kutoa mchango mkubwa katika ustawi wa Taifa kiroho, kiuchumi na kijamii kwani limeweza kuifikia jamii hata katika maeneo ambayo Serikali haijaweza kufikisha huduma hususani vijijini.
Dkt. Mpango ameliasa kanisa kufundisha na kulea vijana katika maadili mema na kuthamini kufanya kazi halali kwani nyakati hizi kuna ongezeko la mmomonyoko mkubwa wa maadili katika jamii ikiwemo ulevi, vitendo vya rushwa, uvivu, wizi na ufisadi, mauaji ya kutisha na idadi kubwa ya ndoa kuvunjika na kuongezeka kwa watoto wa mitaani.
Kwa upande wake Askofu Method Kilaini ameishukuru serikali kwa ushirikiano iliyompatia kwa kipindi chote cha miaka hamsini ya utumishi wake.
Aidha amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa mwaka mmoja wa uongozi wake wenye mafanikio makubwa na kazi nzuri aliyoifanya, na kwamba katika kipindi cha mwaka mmoja wa uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan taifa limeongozwa kwa utu, amani na mshikamano pamoja na hatua mbalimbali za maendeleo kwa wananchi.