Mbunge wa jimbo la Kawe mkoani Dar es Salaam, Askofu Josephat Gwajima amepewa adhabu ya kutohudhuria mikutano miwili ya Bunge baada ya kutiwa hatiani na
Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge.
Bunge pia limevitaka vyombo vya dola vimchukukilie hatua za kisheria Askofu Gwajima kwa kuwa kauli zake ambazo amekuwa akizitoa zina jinai ndani yake na zinahatarisha usalama wa nchi.
Taarifa ya Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge iliyotolewa Bungeni na Mwenyekiti wa Kamati hiyo Emmanuel Mwakasaka imeazimia Chama Cha Mapinduzi (CCM) anachotoka Askofu Gwajima kimchukulie hatua za kinidhamu.
Askofu Gwajima ametiwa hatiani kwa makosa ya kudhalilisha na kushusha nafasi ya Bunge, Wabunge na Viongozi, kuchonganisha mhimili wa bunge dhidi ya mhimili wa Serikali na Wananchi, kuonesha dharau, na kushusha heshima ya bunge, shughuli za bunge na uongozi wa bunge.