Askari sita wa Jeshi la Mali wameuawa na wengine 10 wamejeruhiwa baada ya kutokea shambulio kwenye mji wa Mondoro, shambulio linalodhaniwa kutekelezwa na wanamgambo.
Jeshi la Mali limeeleza kuwa mara baada ya shambulio hilo, askari wake walifanya shambulio la anga katika maeneo yanayokaliwa na wanamgambo hao ikiwa ni kulipiza kisasi na kuharibu mali pamoja na kujeruhi wanamgambo kadhaa.
Mwezi Septemba mwaka 2019 kikundi kimoja cha wanamgambo nchini Mali chenye uhusiano na mtandao wa kigaidi wa al-Qaeda, kiliwaua askari arobaini baada ya kushambulia kambi iliyopo katika mji huo huo wa Mondoro na katika mji mwingine wa Boulkessi.
Hivi karibuni, Rais Ibrahim Boubakar Keita wa Mali alikaririwa akisema kuwa anataka kufanyika kwa mazungumzo baina ya vikundi vya wanamgambo na serikali ili kuzuia mashambulio yanayofanywa katika maeneo mbalimbali ya nchi hiyo na kusababisha vifo.