Asilimia 10 ya watu wanaishi Duniani wanaugonjwa wa figo

0
1306

Asilimia 10 ya watu duniani wanaishi na magonjwa sugu ya figo huku asilimia 50 ya watu wenye umri zaidi ya miaka 75 wana ugonjwa sugu wa Figo.

Hayo yamesemwa na Mganga mkuu wa Serikali Dkt. Aifello Sichalwe wakati wa ufunguzi wa kongamano la kisayansi la wauguzi wataalamu wa Africa lililofanyika jijini Dar es Salaam.

“Dhima ya kongamano hili ni kuleta maendeleo ya huduma ya magonjwa ya figo Duniani ambapo jukumu la elimu na ubunifu kwenye nchi za Afrika na dhima hii imekuja kwa wakati muafaka ambapo Tanzania inaenda kuimarisha na kupanua upatikanaji wa huduma za figo”. Amesema Dkt. Sichalwe

Dkt. Sichalwe amebainisha kuwa Mpaka Janauri 31, 2022 wagonjwa 2,750 nchini Tanzania wanapata huduma ya kusafishwa damu (dialysis) na kufikia tarehe 31 Januari mwaka huu wagonjwa 325 wamepandikizwa Figo.

Aidha Dkt. Sichalwe amesema kwa sasa hospitali zinazotoa huduma ya kusafisha damu nchini ni pamoja na Hospitali ya Taifa Muhimbili, hospitali zote za Rufaa za Kanda (Bugando, KCMC, Benjamin Mkapa, Mbeya) na hospitali za Rufaa za Mikoa ya Kagera, Mwanza, Musoma, Kigoma, Arusha, Iringa na Mtwara.

Kongamano hilo linafanyika kwa siku mbili na kuwakutanisha wauguzi kutoka katika nchi tisa za Afrika ikiwepo Kenya, Uganda, Misri, Rwanda, Sudani ya kusini, Burundi, Ghana, Zambia na wenyeji Tanzania.