Ashauri elimu ya fedha iwafikie wananchi wote

0
169

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Urambo, Grace Quintine, ameishauri Wizara ya Fedha kuhakikisha Watanzania wote nchini wanapatiwa elimu ya fedha itakayowawezesha kufanya maamuzi sahihi katika matumizi ya vipato vyao.

Quintine ametoa ushauri huo alipokutana na Timu ya Wataalamu ya Wizara ya Fedha ambayo ilifika wilayani Urambo mkoani Tabora, kutoa elimu ya fedha kwa wananchi ili waweze kutumia fursa mbalimbali zilizopo katika Sekta ya Fedha na kujikomboa kiuchumi.

“Naamini wananchi wote wakipatiwa elimu hii muhimu ya masuala ya fedha wataweza kuwa na nidhamu ya matumizi lakini pia watakuwa na uelewa wa wapi wakawekeze fedha zao ili kuongeza mitaji katika biashara zao na kuongeza uchumi wa mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla,” alisema Quintine.

Katika zoezi la kutoa elimu kwa wananchi timu ya wataalamu ya Wizara ya Fedha imeambatana na wataalamu kutoka taasisi nyingine za Serikali ikiwemo Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA) ikiwa ni Utekelezaji wa Mpango Mkuu wa Maendeleo ya Sekta ya Fedha kwa mwaka 2021/2022 hadi 2029/2030.