Apandishwa kizimbani kwa kuishi nchini kinyemela

0
190

Mtu mmoja Raia wa Yemen, – Edhah Nahad amepandishwa kizimbani katika mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es salaam, akikabiliwa na mashtaka manne likiwemo la kughushi nyaraka za kuishi nchini kinyume cha sheria.

Nahad amefikishwa katika mahakama hiyo na kusomewa mashtaka na Wakili wa Serikali Shija Sitta mbele ya hakimu Mkazi Mkuu Huruma Shaidi.

Akisoma hati ya mashtaka, Wakili wa Serikali Sitta amesema mshtakiwa huyo anadaiwa kutenda makosa hayo Januari 19 mwaka huu akiwa
Makao makuu ya ofisi za Uhamiaji zilizopo Kurasini Jijini Dar es salaam kinyume na sheria ya Uhamiaji namba 54 ya mwaka 2016 na sheria ya Pasipoti na hati za safari namba 20 ya mwaka 2002.

Katika shtaka la kwanza Wakili Sitta amedai kuwa Januari 19 mwaka huu, maafisa wa Uhamiaji walimkamata mshtakiwa huyo akiishi bila kuwa na kibali cha kuishi nchini.

Kosa la pili ni la kutoa nyaraka za uongo ili kujipatia hati ya kusafiria kinyume cha sheria akiwa katika ofisi za Uhamiaji.

Kosa jingine ni kumdanganya ofisa wa Uhamiaji kwa kujifanya kuwa yeye ni Mtanzania na kutoa fomu ya maombi ya hati ya kusafiria wakati akijua taarifa alizotoa ni za uongo.

Baada ya kumsomea mshtakiwa mashtaka yake na kukiri kosa, Wakili wa Serikali Shija Sitta ameomba mahakama hiyo kutoa adhabu kali kwa mshtakiwa huyo ili iwe onyo kwa watu wengine wenye tabia kama hiyo.

Aidha mshtakiwa huyo ameomba mahakama kumpunguzia adhabu kwa madai kuwa amekimbia vita nchini mwake na kwamba familia inamtegemea.

Hata hivyo hakimu Huruma Shaidi amesema katika kosa la kwanza na la nne ambalo ni la kukutwa akiishi nchini bila kuwa na vibali maalum na mshtakiwa kukiri kutenda makosa hayo, mshtakiwa huyo atapaswa kulipa faini ya shilingi laki tano kwa kila kosa ama kwenda jela mwaka mmoja.

Aidha katika kosa la pili na la tatu ambalo ni la kuwasilisha nyaraka za uongo na kuwadanganya maafisa wa Uhamiaji, Hakimu Huruma amesema mshtakiwa huyo anatakiwa alipe faini ya shilingi laki mbili kwa kila kosa ama kwenda jela miezi nane.

Mpaka Mwandishi wa TBC anaondoka Mahakamani hapo, mshtakiwa huyo alikuwa kwenye taratibu za kukamilisha taratibu zingine za kimahakama kulingana na maamuzi yaliyotolewa na mahakama hiyo.