Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani amemuondoa kazini fundi mchundo wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) wilayani Kisarawe mkoani Pwani, kwa kushindwa kumsimamia mkandarasi anayepeleka umeme katika maeneo ya wilaya hiyo, Wilaya ya Mkuranga na yale yaliyopo pembezoni mwa manisapaa ya Ilala mkoani Dar es salaam.
Waziri Kalemani amechukua uamuzi huo baada ya kutembelea maeneo ya Kivule, Bomba Mbili na Dondwe ili kukagua mradi huo na kushuhudia baadhi ya nguzo zikiwa zimetelekezwa, huku wananchi wakiilalamika serikali kutowapelekea huduma ya umeme.
Ametoa muda wa saa sita kwa mkandarasi huyo kusambaza na kuchimbia nguzo zote zilizotelekezwa, ili zisiendelee kuharibika na pia kumtaka Machi Thelathini mwaka huu awe amefikisha umeme na kuuwasha katika maeneo hayo, vinginevyo atachukuliwa hatua za kisheria.
Mradi huo wa kusambaza umeme katika maeneo ya wilaya ya Kisarawe, wilaya ya Mkuranga na yale yaliyopo pembezoni mwa manispaa ya Ilala, unatekelezwa na Wakala wa Umeme Vijijini (REA) kupitia mpango wa Peri Urban.
Katika ziara hiyo, Waziri Kalemani amekataa kuwasha umeme katika mtaa wa Bomba Mbili uliopo Majohe, baada ya kubaini umeme huo umeunganishwa kwa mtu mmoja na kuwaacha wengine ambao tayari wamekamilisha taratibu zote ili waweze kuunganishiwa umeme.