Baadhi ya wakazi wa Manispaa ya Kigoma – Ujiji wanadaiwa kung’oa nguzo na vibao vya anwani za makazi na kuviuza kama vyuma chakavu.
Katibu Tawala wa Wilaya ya Kigoma, Mganwa Nzota amesema tayari ofisi yake kwa kushirikiana na vyombo vingine vya usalama imeanza msako dhidi ya wahalifu hao ambao wanadaiwa kung’oa anwani hizo za makazi nyakati za usiku.
Nzota alikuwa akizungumza wakati wa mafunzo ya utekelezaji wa mfumo wa anwani za makazi kwa watendaji wa kata, mitaa na wenyeviti wa mitaa katika Manispaa ya Kigoma – Uiji.
Amesema tabia hiyo ya kung’oa nguzo na vibao vya anwani za makazi inakwamisha juhudi za Serikali katika kuboresha mtandao wa anwani za makazi katika wilaya ya Kigoma na hivyo kuwataka wananchi wote kushirikiana katika kutoa taarifa kwa vyombo vya ulinzi na usalama pindi wanapobaini uwepo wa watu wanaojihusisha na vitendo hivyo .