Aliyewadanganya polisi akamatwa

0
245

Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam linamshikilia Deodatus Luhela (35) mhasibu wa kampuni ya Your Home Choice iliyopo eneo la Keko mkoani Dar es Salaam, kwa tuhuma za kutoa taarifa za uongo.

Kamanda wa polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Muliro Jumanne amesema kuwa tarehe 14 mwezi huu Luhela alifika kituo kidogo cha polisi cha Gongo la Mboto na kudai kuwa majambazi wamemjeruhi na kumpora shilingi milioni 60 alizotumwa na mwajiri wake kuzichukua kutoka benki ya CRDB tawi la Tazara.

Amesema katika maelezo yake polisi Luhela alidai kuwa, majira ya saa 3:30 asubuhi tarehe 14 mwezi huu alivamiwa na majambazi wawili waliokuwa na gari nyeusi baada ya kumtishia kwa silaha na baadaye walimuingiza ndani ya gari ambapo walimjeruhi mkono wa kushoto na shavuni na kumpora fedha alizokuwa nazo.

Luhela alisema baadaye walimtupa maeneo ya Gongo la Mboto njia panda ya Pugu na Mbezi ambapo alijikongoja hadi katika kituo hicho kidogo cha polisi cha Gongo la Mboto.

Makachero wa Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam walipomuhoji mtu huyo walibaini taarifa hizo zilikuwa ni za uongo, na siku iliyofuata aliwaongoza askari hadi Chanika Kitunguu alipokuwa amezificha pesa hizo.

Kufuatia tukio hilo, Kamanda Muliro amewatahadharisha wananchi juu ya tabia ya kutoa taarifa za uongo kwa maafisa wa Serikali.

Amesema kitendo hicho ni kosa na mtu yeyote atakayebainika kutoa taarifa hizo za uongo atachukuliwa hatua stahiki kwa mujibu wa sheria ikiwa ni pamoja kufikishwa mahakamani.