Aliyeua bila kukusudia kisa shilingi Elfu sita aachiwa kwa masharti

0
278

Mahakama ya Kuu Kanda ya Dar es Salaam imemwachia huru mfanyabiashara Steven Aloyce mkazi wa Vingunguti kwa masharti ya kutotenda kosa la jinai kwa kipindi cha mwaka mmoja.

Uamuzi huo umetolewa na Jaji wa mahakama hiyo Leila Mgoya baada ya mfanyabiashara huyo kukiri kosa la kumuua mwenzake Kijuba Mwangu bila kukusudia.

Kabla ya kutolewa kwa uamuzi huo wa kesi namba 44 ya Mwaka 2019 wakili Mwandamizi wa Serikali Janeth Magoho amedai Oktoba 16, mwaka 2017 mshitakiwa huyo alitekeleza mauji hayo kwa kumchoma kisu cha mgongoni na kifuani Kijuba, akiwa eneo la Vingunguti machinjioni kwa madai ya marehemu kumchukilia shilingi elfu sita na kukimbia nayo akidai ni ya kwake.

Aidha Wakili Magoho amedai baada ya marehemu kuchomwa kisu aliomba msaada kwa wasamaria wema ambao walimkimbiza katika Hospitali ya Amana lakini hata hivyo baada ya kufikishwa iligundulika ameshafariki dunia kabla ya kufikishwa Hospitalini.

Katika utetezi wake mshitakiwa huyo amekiri kumuua mwenzake bila kukusudia hivyo kuomba mahakama impunguzie adhabu kwa madai ya kukaa gerezani kwa muda wa miaka mitano na kwamba anajutia kutenda kosa hilo nakuahidi kuwa mfano bora kwenye jamii pasi kurudia kosa.

Akitoa uamuzi wake Jaji Mgoya amesema amezingatia mazingira ya kosa lilipotendeka kwamba ni mazingira ya machinjioni ambayo kisu hakiwezi kukosekana licha ya kwamba mshitakiwa angeweza kutawala hasira zake ili kuzuia madhara yasitokee.

Pia ameeleza kwamba amezingatia muda ambao mshitakiwa amekaa Gerezani tangu alipokamatwa hivyo anaamini amejifunza na kujutia makosa yake hivyo kuachiwa kwa masharti hayo yaliyotajwa sambamba na kuwa chini ya uangalizi maalumu kwa kipindi cha mwaka mmoja pasi kutenda kosa la jinai.