Akamatwa akisafirisha Wahamiaji

0
259

Idara ya Uhamiaji mkoani Mbeya inamshikilia Enock Moses mkazi wa mkoa wa Dar es Salaam, kwa tuhuma za kusafirisha wahamiaji 12  raia wa Ethiopia.
 
Ofisa Uhamiaji wa mkoa wa Mbeya, Kigongo Shille amewaambia Waandishi wa habari jijini Mbeya kuwa,  Enock ambaye ni dereva aliahidiwa kulipwa shilingi milioni 1.2 endapo angewafikisha wahamiaji hao mkoani Mbeya wakitokea Chalinze mkoani Pwani.


 
Amedai kuwa Enock alikuwa akiwasafirisha Wahamiaji hao kwa kutumia lori lenye namba za usajili T 453 DJQ na kuwaficha chini ya vifaa mbalimbali vya ujenzi ikiwa ni pamoja na mbao.
 
“Kuna mtu jina limehifadhiwa, ambaye ndio alimpatia kazi ya kuwasafirisha kwa ujira wa shilingi milioni 1.2 akifanikiwa kuwafikisha Mbeya ambako tayari kuna mtu mwingine aliandaliwa kuwachukua na kuwatafutia usafiri wa kuelekea Tunduma mkoa wa Songwe ili wavuke mpaka wa nchi jirani wa Zambia waende Afrika Kusini na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo.” amesema Shille
 

Amesema Enock amekamatwa baada ya askari wa uhamiaji waliokuwa doria kwenye kituo cha ukaguzi kata ya Inyara wilaya ya Mbeya kutilia shaka lori hilo na kulisimamisha.  na baada ya ukaguzi wakabaini kuwepo kwa Wahamiaji hao.
 
Ofisa huyo wa  Uhamiaji wa mkoa wa Mbeya amesema kwa sasa uchunguzi unaendelea, ili kubaini mtandao unaojihusisha na biashara ya kuingiza nchini wahamiaji kutoka mataifa mengine.