Ajenda ya kutokomeza Malaria iwe ya kudumu

0
129

Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel amezitaka Kamati za Usalama kuona umuhimu wa kuifanya ajenda ya kutokomeza Malaria iwe ya kudumu kwenye vikao vya maamuzi.

Dkt. Mollel ameyasema hayo akiwa amemwakilisha Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu kwenye kilele cha Siku ya Malaria Duniani iliyofanyika mkoani Tabora na kusema kuwa Tanzania imeendelea kupiga hatua katika vita dhidi ya Malaria ikilinganishwa na miaka zaidi ya ishirini iliyopita ambapo maambukizi na vifo vya ugonjwa huo vilikuwa kati ya asilimia 45 hadi 50.

Aidha, Dkt. Mollel amesema azma ya Serikali ni kufikia asilimia 3.5 ifikapo mwaka 2025 na kuwa na ziro Malaria 2030 huku akisisitiza kwa kusema kuwa itafikiwa endapo juhudi za makusudi zitafanywa kwa ushirikiano baina ya Serikali na wadau.

Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia Afya kutoka Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali.za Mitaa (TAMISEMI) Samsoni Maella, amesema utumiaji wa mifumo ya GoTHOMIS na FFARS umekuwa chachu ya kukusanya takwimu sahihi kwa ajili ya ngazi ya maamuzi, hali iliyochangia kufanya maamuzi sahihi kutokana na kuwa na takwimu sahihi.