Watu 10 wamefariki dunia na mmoja amejeruhiwa katika ajali ya gari iliyohusisha gari dogo la mizigo aina ya Suzuki Carry maarufu Kirukuu na lori la Polisi, iliyotokea katika eneo la Dutch Conner wilaya ya Siha mkoani Kilimanjaro.
Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa amesema watu hao wamefariki dunia wakati wakielekea sokoni katika eneo la Ngarenairobi.
Amesema awali dereva wa ‘Kirukuu’ alikamatwa kwa kosa la kupakia abiria kinyume cha sheria na kutozwa faini, lakini alipofika kituo kinachofuata alipakiza abiria wengine.
Kamanda Maigwa amesema miongoni mwa watu hao 10 waliofariki dunia ni askari wa Jeshi la Polisi namba G 8813 Denis Mamkwe kutoka Shule ya Polisi Moshi.
Miili ya watu waliofariki dunia katika ajali hiyo imehifadhiwa katika hospitali ya Kibong’oto iliyopo wilayani Siha.