Ajali ya barabarani yagharibu maisha ya watu 14 Singida

0
525

Watu 14 wamefariki dunia na wengine watatu wamejeruhiwa katika ajali  ya barabarani iliyohusisha basi dogo aina ya hiace na lori katika eneo la Mkiwa wilayani Manyoni mkoani Singida.

Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Singida, -Sweetbert Chawike amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo usiku wa kuamkia hii leo na kuongeza kuwa basi hilo dogo lilikuwa likitokea mkoani Mwanza likielekea Itigi mkoani Singida na lilikuwa limebeba abiria waliokuwa wakielekea kwenye sherehe za harusi.

Kamanda Chawike amesema lori lililogongana na basi hilo dogo lilikuwa likitoka jijini Dar es salaam na lilikuwa likielekea Kahama mkoani Shinyanga.

Amesema uchunguzi wa awali onaonesha kuwa chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa dereva wa hiace ambaye alitaka kulipita gari jingine pasipo kuchukua tahadhari.

Majeruhi watatu wa ajali hiyo wanaendelea kupatiwa matibabu katika hospitali ya mkoa wa Singida na miili ya watu wote waliofariki dunia
katika ajali hiyo imehifadhiwa katika hospitali hiyo.