Airbus yatua Songwe

0
144

Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Atupele Mwakibete amesema, kuanza kutua kwa ndege aina ya Airbus katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Songwe kutaendelea kuifungua nchi na ni fursa kwa wafanyabiasara hasa wa Nyanda za Juu Kusini na wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).

Mwakibete ameyasema hayo mara baada ya kupokea ndege aina ya Airbus yenye namba A220-300, mali ya Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL), iliyotua kwa mara ya kwanza katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Songwe kwa ajili ya majaribio ya uwanja huo.

Amesema ndege hiyo imefanya majaribio ya kutua katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Songwe baada ya uwanja huo kutanuliwa njia zake ili kupokea ndege kubwa na kuwekwa taa zitakazowezesha ndege hiyo kufanya safari usiku.

Kwa upande wake mkuu wa mkoa wa Mbeya, Juma Homera amesema, kutua kwa ndege kubwa katika uwanja huo wa ndege wa Kimataifa wa Songwe ni mafanikio makubwa ya serikali ya awamu ya sita mkoani humo kutokana na mazao mbalimbali yanayolimwa mkoani humo.

Ndege hiyo imewasili uwanjani hapo ikiwa na abiria waliofika mkoani Mbeya kwa ajili ya sherehe za wakulima maarufu Nanenane.