Ahukumiwa na mahakama kwa kumjeruhiwa mwanamke jicho kwa kiatu

0
446

Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam imempa adhabu ya kuhudumia jamii na kulipa fidia ya shilingi milioni 7 mfanyabiashara Focus Munisi, mkazi wa Manispaa ya Morogoro baada ya kutiwa hatiani kwa kosa la kumsababishia madhara na ulemavu wa kudumu wa jicho Nanjiava Geofrey.

Hukumu hiyo imetolewa na Jaji wa Mahakama Kuu, Laila Mgonya kupitia kikao cha mahakama hiyo kilichofanyika katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Morogoro baada ya kuridhishwa na ushahidi uliotolewa na upande wa Jamhuri na kuthibitisha kuwa mfanyabiashara huyo alimpiga mwanamke huyo kwenye jicho la kulia kwa kutumia kiatu chenye kisigino kirefu hali iliyosababisha kutolewa kwa jicho lake.

Kesi hiyo iliyowakilishwa na wakili wa serikali Kalistus Kapinga na Veronica Chacha waliiomba mahakama kutoa adhabu kali kwa mshtakiwa kwa kitendo hicho ili iweze kuwa fundisho kwa watu wengine.

Nao upande wa utetezi ambao umewakilishwa na wakili Benjamin Jonas na Hadija Shabani umeomba mahakama kutoa adhabu ya huruma kwa mteja wao kwa kuwa ni kosa lake la kwanza na anasumbuliwa na ugonjwa wa kisukari pamoja na shinikizo la damu huku bado familia ikiendelea kumtegemea akiwemo mama yake mzazi.

Mshtakiwa huyo alitenda kosa hilo Septemba 15 mwaka 2016 akiwa katika ofisi iliyopo ndani ya hotel yake inayojulikana kwa jina la Tax Pares iliyopo Manispaa ya Morogoro.