Ahukumiwa miaka 60 jela kwa kumbaka na kumlawiti mtoto

0
195

Mahakama ya Wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam imemhukumu Joseph Moyo, mkazi wa Goba, kifungo cha miaka 60 jela baada ya kutiwa hatiani kwa makosa mawili ya ubakaji na kulawiti.

Hukumu hiyo imetolewa na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Kinondoni, Frank Mushi baada ya kujiridhisha na ushahidi uliotolewa na mashahidi sita.

Kabla ya kutolewa kwa hukumu hiyo, Wakili wa Serikali, Shindai Michael ameiambia mahakama kuwa mshitakiwa huyo alitenda makosa hayo katika tarehe tofauti kati ya Mei 2018 na Julai 29, 2018 eneo la Goba Kibuhulu, Wilaya ya Kinondoni.

Aidha, katika shitaka la kwanza na pili Wakili Michael amesema katika tarehe hizo mshitakiwa huyo alimbaka na kumlawiti mtoto wa miaka 15 katika eneo la Goba Kibuhulu.

Kesi hiyo ya jinai iliyokuwa na mashahidi sita wa upande Jamhuri na utetezi, kwa mara ya kwanza ilitajwa Mahakamani hapo mwaka 2018.