Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe amesema kuanzia mwaka 2024 nchi zote za Afrika zitapata mialiko ya kuhudhuria maonesho na shereha ya Kimataifa ya wakulima Nanenane.
Akizungumza katika Sherehe na Maonesho ya Kimataifa ya Wakulima Nanenane mkoani Mbeya yaliyofunguliwa rasmi hii leo, amesema mialiko hiyo haitahusisha viongozi peke yake kuhudhuria bali hadi wakulima na wanunuzi wa mazao katika nchi hizo watapata mialiko hiyo.
Bashe ameongeza kuwa kufuatia kupanda hadhi kwa maonesho ya Nanenane kutoka kuwa ya kitaifa na kuwa ya kimataifa, juhudi mbalimbali zinaendelea ikiwemo utekelezaji wa maelekezo ya Serikali ya kuboresha maeneo yanayotumika kwa ajili ya sherehe hizo kwa kuyajenga ili yawe ya kudumu, yaakisi hadhi ya kimataifa.
Aidha, amesema kuwa kiwanja cha John Mwakangale kilichopo mkoani Mbeya kitakuwa moja ya viwanja vya kudumu katika mikoa ya nyanda za juu kusini kwa ajili ya maonesho Kimataifa ya wakulima Nanenane.