African Media Group mambo poa

0
1055

Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa Rais John Magufuli amefanya ziara fupi ya kutemblea ofisi za kampuni ya African Media Group inayomiliki vituo vinne vya Televisheni na viwili vya Redio.

Akizungumza na Menejimenti pamoja na Wafanyakazi wa kampuni hiyo jijini Dar es salaam ikiwa ni sehemu ya sherehe za miaka 42 ya kuzaliwa kwa Chama Cha Mapinduzi, Rais Magufuli amewapongeza wafanyakazi hao kwa utendaji kazi wao mzuri na kuwataka kufanya kazi kibiashara.

Rais Magufuli ameahidi kutatua changamoto mbalimbali zinazoikabili kampuni hiyo ikiwemo ile ya uchakavu wa vifaa na majengo na kuahidi kununua vifaa vipya ili kuviwezesha vyombo vya habari vinavyomilikiwa na kampuni hiyo ya African Media Group kuonekana nchi nzima.

Kuhusu ubovu na ufinyu wa jengo linalotumika hivi sasa, Rais Magufuli ameiagiza Menejimenti ya kampuni  hiyo pamoja na wafanyakazi kushirikiana ili kutafuta jengo katika sehemu watakayohitaji ili liweze kuandaliwa kama ofisi.

Akiwa katika ofisi hizo Rais Magufuli ameahidi kutoa Shilingi Milioni Mia mbili kwa ajili ya kununua vifaa mbalimbali ikiwa ni pamoja na Camera ambazo zitasaidia kurahisisha utendaji kazi katika vituo mbalimbali vya televisheni vilivyo chini ya kampuni hiyo ya African Media Group, kampuni inayomilikiwa na CCM.