Aeleza Bukoba ilivyonufaika miaka 3 ya Samia

0
197

Zaidi ya shilingi bilioni 15 zimetolewa na serikali kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo katika Manispaa ya Bukoba mkoani Kagera na kuchangia ukuaji wa sekta mbalimbali za kijamii na kiuchumi.

Hayo yamebainishwa na Mbunge wa Jimbo la Bukoba Mjini, Stephen Byabato wakati akiwahutubia wananchi wa Manispaa ya Bukoba kwenye Mkutano wa hadhara uliofanyika katika Viwanja vya Soko Kuu la Manispaa hiyo.

Byabato amesema kuwa katika miaka mitatu ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan serikali imetoa fedha nyingi ambazo zimesaidia kuboresha mindombinu ya elimu, barabara, huduma za afya na shughuli za uchumi kwa wakazi wa Jimbo la Bukoba Mjini.

Amesema kupitia fedha hizo baadhi ya maeneo ambayo hayakuwa na shule yamepata shule mpya za msingi na sekondari sambamba na kuanzishwa kwa huduma za viwanda, biashara na uwekezaji.

Ametaja manufaa mengine kwa wana-Bukoba kuwa ni uwekaji wa taa za barabarani, marekebisho katika soko kuu, usafishaji Mto Kanoni, ujenzi wa Hospitali ya Wilaya iliyopo Nshambya pamoja na uunganishaji umeme kwa wananchi kupitia miradi inayotekelezwa na Wakala wa Umeme Vijijini (REA).

Kutokana na hayo, Wakili Byabato amewahimiza wananchi kuendelea kushirikiana na serikali katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.