Adaiwa kuiba mtoto ili kuwaridhisha wakwe

0
290

Jeshi Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limemkamata Mariam Renatus (22) kwa tuhuma za kuiba mtoto mwenye umri wa miezi 10 Miracle Ayoub eneo la Gongo la Mboto, Dar es Salaam na kwenda naye hadi kijiji cha Bugalama mkoani Geita.

Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro amesema Polisi walipokea taarifa za kuibwa kwa mtoto huyo Februari 06, 2024 majira
ya saa moja usiku kutoka wa mama wa mtoto huyo aliyefahamika kwa jina la Victoria Charles
(34) mkazi wa Gongo la Mboto.

Amesema mtuhumiwa huyo wa wizi alijifanya msaidizi wa kazi na baadae kupata fursa ya kumuiba mtoto huyo.

Uchunguzi wa awali wa Jeshi la Polisi umebaini kuwa mtuhumiwa alimuiba mtoto huyo kwa lengo la kuwaridhisha wakwe zake baada ya kuwadanganya kuwa alijifungua mtoto tangu mwezi wa Mei mwaka 2023 baada ya kuwa na mahusiano na kijana wao.

Mtoto amepatikana akiwa na afya njema na mtuhumiwa huyo atafikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazomkabili.