Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Daniel Chongolo amewataka Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) kuchangamka kununua mahindi kwa wakati ili kuwafanya wakulima kuendelea na shughuli zao za maendeleo.
Katibu Mkuu ameyasema hayo Ruvuma wilayani Mbinga wakati akiongea na wananchi na wanachama wa chama hicho wakati wa ziara ya wajumbe wa Sekretarieti ya Halmashauri kuu ya CCM Taifa ambapo amesema, tayari Rais Samia Suluhu Hassan ametoa kiasi cha shilingi bilioni 50 kwa ajili ya ununuzi wa mahindi hayo kwa awamu ya pili.
Chongolo amewaambia NFRA kuelekeza fedha hizo katika kazi husika kwani kazi ya fedha si kukaa mifukoni au kwenye akaunti za Taasisi, kazi yake ni kuelekea kwenye maeneo yaliyokusudiwa.
“Mwananchi amelima shamba lake kwa bidii, kavuna vizuri mazao yake anataka kutengeneza mambo yake na anataka kujipanga na pembejeo za msimu ujao wakicheleweshwa kwenye mambo ya Msingi watakuwa hawatendewi haki.
“Sisi tufanye kazi yetu ya msingi tununue mahindi kwa wakati, mahindi yakishanunuliwa mwananchi atajipangia mwenyewe manunuzi yake kwa sababu fedha ni ya kwake mwenyewe,” amesisitizaChongolo.
Katika hatua nyingine, Katibu Mkuu amewaomba wananchi wa Mbinga kulima mazao mengine ambayo yanastawi vyema mkoani humo ili kuendeleza kupanua wigo wa mzunguko wa kipato.