Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Jenerali Venance Mabeyo, amewasamehe Vijana 854 waliokuwa wakifanya mafunzo katika kambi mbalimbali za Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) na kufukuzwa mwezi Aprili mwaka 2021 kutokana na utovu wa nidhamu.
Taarifa hiyo imetolewa mkoani Dar es Salaam na Kaimu Mkurugenzi wa Habari na Uhusiano wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) Luteni Kanali Gaudentius Ilonda wakati wa mkutano wake na Waandishi wa habari.
Luteni Kanali Ilonda amesema msamaha huo umetolewa baada ya JWTZ kufanya uchunguzi wa kina na kujiridhisha kwamba Vijana hao walifanya vitendo vya utovu wa nidhamu kwa sababu ya utoto, kwa kutojitambua, kurubuniwa na wengine walifanya kwa kufuata mkumbo.
“Kuna baadhi ya Watanzania ambao walishiriki kuwarubuni Vijana hawa naomba tuache vitendo vya kuwarubuni tuache Vijana wapate mafunzo yao ya stadi za maisha ili waje kulitumikia Taifa lao kwa moyo mmoja.” amesema Luteni Kanali Ilonda
JWTZ imeongeza kuwa kuna taarifa kuwa kijana mmoja kati ya 854 waliofukuzwa amefariki dunia na walio hai ni 853, hivyo imeamuriwa Vijana wote 853 warudi makambini.