Zimbabwe wanapiga kura leo

0
372

Raia wa Zimbabwe leo wanapiga kura kumchagua Rais pamoja na Wabunge, baada ya kuhitimishwa kwa kampeni za uchaguzi huo ambazo zilitawaliwa na suala la mfumko wa bei.

Kutokana na zoezi hilo la upigaji kura, leo ni siku ya mapumziko nchini Zimbabwe ili kuwawezesha wapiga kura Milioni 6.62 waliojiandikisha kupata nafasi ya kupiga kura.

Rais wa sasa wa Zimbabwe, Emmerson Mnangagwa kutoka
chama tawala cha Zanu-PF
anawania kiti hicho huku akikabiliwa na upinzani kutoka wagombea wengine 10 akiwemo Nelson Chamisa kutoka chama kikuu cha upinzani cha Citizens Coalition for Change (CCC).

Mshindi wa kiti cha urais katika uchaguzi huo atalazimika kupata zaidi ya asilimia hamsini ya kura zote zilizopigwa na na ikiwa hakutakuwa na mshindi, duru ya pili ya uchaguzi itafanyika baada ya wiki sita toka kutangazwa kwa matokeo.

Huo ni uchaguzi wa kwanza tangu kifo cha aliyewahi kuwa Rais wa Zimbabwe, Robert Mugabe mtu ambaye alitawala siasa za Zimbabwe na chama tawala cha Zanu-PF kwa miongo kadhaa.

Alifariki dunia mwaka 2019 takribani miaka miwili baada ya kuondolewa madarakani katika mapinduzi ya kijeshi na nafasi yake kuchukuliwa na Naibu wake Emmerson Mnangagwa.